Iringa Mjini, saa kumi na mbili na nusu jioni. Ni Jumapili. Ni Sikukuu ya Pasaka. Ona bucha hiyo ya nyama, ' Executive Butcher'. Mwone mama huyo mwenye haraka. Mwingine angedhani, kuwa siku hii ni yenye pilika nyingi.
Hapana, si kila mahali. Ninapopiga picha hiyo nimesimama kwenye meza ya magazeti, mwuzaji anaitwa Salumu. Hakuna mteja mwingine, ni mimi tu, na mwuzaji. Na mie sijafika mjini tangu asubuhi, nimekuja kuchungulia vichwa vya habari.
Ndio, mahali hapaniliposimama ni karibu na Soko Kuu, lakini kuna ukimya mkubwa. Wanaotembea mitaani wanahesabika. Ndio, kuna ombwe fulani hivi- vacuum.
Siku kama ya leo kwa wengine ni yenye mkanganyiko mwingi. Ni mkanganyiko wa kimaisha. Uliye Ughaibuni, au hata uliye Tanzania lakini uko mbali na hali halisi, huenda usielewe ni kwanini bucha hiyo iko wazi mpaka giza linapoingia, tena kwenye Jumapili ya Pasaka.
Mwenye bucha anaielewa jamii inayomzunguka. Hajakosea. Siku kama ya leo kuna baba au mama aliyewaacha watoto nyumbani wakisubiri aende akahangaikie nyama ya pasaka. Hata kama kila siku familia inakula ugali na maharage au mboga za majani, basi, walau siku kama ya leo nyama iliwe, si Pasaka!
Lakini kilo ya nyama imefikia elfu nne. Leo si siku ya kurudi nyumbani na nusu kilo ya utumbo. Na mzazi huyu amehangaika wiki nzima kutafuta hela ya Pasaka. Huenda kuna baba au mama aliyeahidiwa elfu hamsini jana jioni. Kaifuata, hakuipata. Kaambiwa arudi leo mchana. Ikafika mchana, kaambiwa arudi saa kumi na moja jioni. Bahati, ameipata, elfu hamsini.
Huyoo, ataanza mwendo kuitafuta bucha ya nyama. Kama hakuna wenye bucha waelewa kama mwenye ' Executive Butcher', basi, kuna familia nyingi, siku kama ya leo zingeipitisha kwa kula ugali na maharage, kwa vile, bucha zote zimefungwa saa sita mchana!
Nilipata kuandika, kuwa watu wa Ulaya na Marekani wanajua zaidi namna Waafrika tunavyokufa. Si wanasoma kwenye magazeti na kuona kwenye runinga, lakini hawajui jinsi tunavyoishi. Na watashangaa sana kuona ' Executive Butcher' iko wazi mpaka saa moja usiku, siku ya Pasaka!
Maggid,
Iringa.
Jumapili, Aprili 24, 2011
0 Yorumlar